Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) lilifanikiwa kuitisha mkutano mkuu maalumu uliofanyika tarehe 17 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Four Points Hotel, Jijini Dar es Salaam. Mkutano huu ulihudhuriwa na wanachama kutoka sekta mbalimbali za kilimo pamoja na wadau muhimu, na ulijikita katika kufanya uchaguzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi kufuatia kumalizika kwa muda wa Bodi iliyokuwepo kwa mujibu wa Katiba ya Baraza.
Katika Mkutano huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake, Dkt. Jacqueline Mkindi, alipata nafasi ya kutoa hotuba ya kuaga. Akiwashukuru wanachama wote kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kulitumikia Baraza, Dkt. Mkindi alieleza mafanikio muhimu yaliyopatikana chini ya uongozi wake. Mafanikio hayo yalijumuisha:
• Kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na wadau wa sekta ya kilimo.
• Kukuza sauti ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo kupitia ushawishi wa sera bora.
• Kuboresha mifumo ya ndani ya utendaji kazi wa Baraza.
Aidha, aliwahimiza wanachama kuendelea kushikamana, kuthamini mafanikio yaliyopatikana, na kuunga mkono Bodi mpya kwa ari na mshikamano ili kuendeleza mafanikio ya Baraza na ustawi wa kilimo nchini. Katika uchaguzi uliofanyika, Bw. Jitu Soni alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya ACT. Akihitimisha Mkutano huo kwa hotuba yake ya shukrani, Bw. Soni aliwashukuru wanachama kwa kumuamini na kuahidi kuwa yeye pamoja na Bodi mpya watafanya kazi kwa bidii, uwazi, na ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha Baraza linaendelea kuimarika na kufikia malengo yake. Mwenyekiti mpya alieleza kuwa vipaumbele vya Baraza katika kipindi kijacho vitajikita katika:
• Kuimarisha ushirikiano na mshikamano baina ya wanachama.
• Kuongeza ushawishi wa kisera kwa manufaa ya sekta ya kilimo.
• Kukuza huduma kwa wanachama na kuongeza thamani ya uanachama.
• Kuwezesha na kuibua fursa mpya za maendeleo katika kilimo.
Baraza la Kilimo Tanzania linatoa pongezi kwa wajumbe wote wapya wa Bodi ya Wakurugenzi na linawashukuru kwa dhati wajumbe waliomaliza muda wao kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Baraza. ACT itaendelea kuwa jukwaa shirikishi lenye nguvu, linalowezesha wakulima na wadau wa kilimo kushiriki kikamilifu katika mabadiliko chanya ya sekta ya kilimo nchini.
Event Date | 04-17-2025 5:00 pm |
Event End Date | 04-17-2025 1:00 pm |
Capacity | Unlimited |
Registered | 40 |
Individual Price | Free |
Location | Online |